ELIMU BORA AU BORA ELIMU

Kwa kiasi kikubwa serikali imejitahidi kutengeneza mazingira ambayo yatamfanya kila mtanzania aweze kwenda shule, ili aweze kujua kusoma na kuandika. Hii ni mojawapo ya njia ya kupambana na maadui wakubwa watatu wa maendeleo katika nchi yetu ambao Hayati Mwalimu Nyerere aliwaweka wazi kuwa ni Maradhi,Ujinga na Umaskini.
Swali ninalojiuliza. Je mikakati au mazingira yaliyowekwa ili kupambana na adui huyu Ujinga, Je yanakidhi vigezo vya kumwangamiza adui huyu katika akili za watanzania? Au elimu inayotolewa ni elimu bora au bora elimu?
Matokeo ya kidato cha nne yametangazwa hivi karibuni na wenye mamlaka ya kutangaza. Wanaohusika wakidai kuwa kiwango cha kufaulu kimepanda bila kutoa maelezo ya kina kimepanda kwa asilimia ngapi tofauti na miaka iliyoyopita. Huu ni ubabaishaji. Kiwango kilichopanda ni kiwango ni kiwango cha watahiniwa waliojiandikisha kufanya mtihani wa kidato cha nne kwa asilimia 30.46 tofauti na mwaka jana. Hi imetokana watahiniwa hawa kutochujwa katika mtihani wa kidato cha pili, ambapo imepelekea matokeo ya mwaka huu kuwa mabaya. Wale wote waliofèli katika mtihani huu ndio wale ambao hawakuwa na sifa za kuendelea na kidato cha tatu, ila waliendelea kwa sababu serikali iliwaruhusu. Matokeo ya uamuzi huo mbovu ndio umeonesha madhara yake katika matokeo haya. Mfano katika shule moja waliofeli kidato cha pili walikuwa 29, lakini waliofeli kidato cha nne ni 25. Kwa matokeo haya baadhi ya vyombo vya habari vikiripoti kuwa matokeo ya mwaka huu ni JANGA LA TAIFA
Swali ninalojiuliza kwa matokeo haya, je hawa waliofeli ambao ni karibu nusu ya waliojiandikisha Je watakwenda wapi?
Baada ya Hayati Mwalimu Nyerere kuchukua nchi kutoka kwa wakoloni, serikali ilianzisha sera ya ujamaa na kujitegemea. Sera hii ilipelekea serikali kutaifisha shule zote za binafsi na kuwa mali ya serikali. Chini ya Hayati Mwalimu Nyerere serikali iliöngeza masomo ya ujuzi mbalimbali,ili mwanafunzi anapomaliza masomo yake aweze kujiajiri mwenyewe hata kama akikosa ajira serikalini au katika kampuni binafsi. Mfano shule za kilimo kama; Machame girls, Gallanos, Malangali, Mpwapwa na nyinginezo. Je elimu hii bado inaendelea kutolewa. Jibu ni hapana. Sasa hawa watahiniwa waliofeli wataelekea wapi? Na hao waliofaulu watafika chuo kikuu, Je baada ya kumaliza chuo kikuu wataelekea wapi endapo baadhi yao watakosa ajira. Serikali hii ya awamu ya nne inatoa elimu bora au bora elimu?
Serikali inajenga shule nyingi za kata inawalazimisha wazazi wawapeleke watoto wao shule. Je huko shuleni wanaenda kufundishwa nani,wanatumia vifaa vipi ili kuweza kujifunza. Unakuta shule wanafunzi wanakaa chini hapohapo shule hiyo ina waalimu wawili toka kidato cha kwanza mpaka cha nne,halafu mwisho wa siku serikali inasema kiwango cha kufaulu kimepanda. Hivi kwa nini serikali inatufanya sisi wananchi wapumbavu?
Serikali irudi nyuma na kuangalia mikakati ya kuinua kiwango cha elimu ilyowekwa na Hayati Mwalimu Nyerere enzi za utawala wake. La sivyo itafika siku nchi hii ni nchi ya wajinga kuanzia Rais mpaka mwananchi wa chini. Na kuendelea kufaidisha wenye akili wachache kama wamiliki wa kampuni hewa ya DOWANS

No comments:

Post a Comment