Sunday, November 20, 2011

WAHITIMU WA MAFUNZO YA UALIMU 2011

Mhe. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, Kwanza tunaomba kukupa pole kwa majukumu mazito uliyonayo katika ujenzi wa taifa letu. Pia tunakupongeza kwa uimara na ushupavu wako katika kusimamia masuala mbalimbali ya Elimu nchini.

Mhe. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, lengo kuu la waraka huu kwako ni kukufikishia lalamiko letu moja kwa moja. Sisi ni wahitimu wa mafunzo ya ualimu tangu mwezi wa tano, mpaka hivi leo ni miezi zaidi ya mitano inaelekea sita bado hatujui mstakabali wetu kuhusu kupatiwa ajira. Katika shule nyingi za serikali, mambo si shwari hata kidogo. Kuna upungufu mkubwa wa walimu wenye ujuzi wa kufundisha. Ni jambo la kusikitisha kuwa walimu wenye cheti, stashahada na shahada kutoka vyuoni hawajaweza kuajiriwa. Baadhi yetu tunabangaiza ilimradi mkono uingie kinywani.

Zimetoka habari mbalimbali katika vyombo vya habari zinazoleta mkanganyiko na sisi kushindwa kuelewa mstakabali wa ajira zetu, utakuwa vipi. Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi la tarehe 06 November. "NAIBU Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala Za Mikoa na Serikali za Mitaa (JUMANNE SAGINI) alisema kuwa ajira tayari zimekamilika na wamepokea majina ya wahitimu 23,027 na kwamba ifikapo November 15 mwaka huu, ajira za walimu hao zitakuwa zimetangazwa. Lakini tarehe hiyo imepita na hakuna kilichotangazwa, sasa tunashindwa kuelewa, Je huyu kiongozi alidanganya umma?

Wakati hilo likiendelea Gazeti la HabariLeo la tarehe 13 November likaandika, "NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, (PHILIPO MULUGO) amesema Serikali itaajiri walimu wapya 23,000 katika kipindi cha mwaka ujao wa fedha." Sasa hapa tunachanganyikiwa, mwaka wa fedha unaanza Julai 2012. Sasa tuelewe lipi kila kiongozi anasema lake. Mhe. Waziri tunaomba utoe tamko rasmi kuhusu swala hili.

Mh. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, tunatumaini kuwa lalamiko,kilio na ombi letu utalipokea na kulifanyia kazi. Tunakutakia afya tele na mafanikio katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa letu na kuinua kiwango cha elimu nchini.


Ahsante sana

No comments:

Post a Comment