Nchi nyingi barani Afrika hupigana ili kuilinda raslimali zao dhidi ya wachache wenye nguvu wanaohitaji kujinufaisha pamoja na mabepari katika nchi za Ulaya na Amerika.
Cha kushangaza Tanzania ni nchi pekee yenye amani ambayo raslimali zake huporwa kimyakimya huku wananchi wake wakilifahamu hilo au kutolifahamu na kutoleta upinzani wowote ili kulinda raslimali zao. Viongozi wa kisiasa na watu wenye uwezo kiuchumi,wamewafanya watanzania kuwa mambumbumbu mzungu wa reli,wasiofahamu lolote kuhusu kuhoji raslimali za nchi yao.
Enzi za utawala wa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,ilikuwa ni vigumu kwa mwanasiasa au mfanyabiashara kuwa na matumizi makubwa tofauti na mshahara wake. Lakini hivi sasa ni kawaida kwa mwanasiasa au mfanyabiashara kuwa na pesa zaidi ya bajeti ya nchi yake.
Jukwaa la siasa limekuwa ndio ngazi au daraja la watu kuweza kujipatia mabilioni na kutumia nguvu ya kisiasa kukwepa kodi. Hivi sasa mtu akiwa na nguvu ya kiuchumi ni lazima atafute nguvu ya kisiasa ili aweze kuendeleza uchumi wake kwa kupindisha sheria na hatimaye kuwa na maamuzi serikalini, na wakati mwingine kufikia hatua ya kuamuru vyombo vya dola kutumia nguvu ili kulinda maslahi yake. Kwa mtindo huu watanzania tunaelekea wapi?
Tumeona yaliyotokea Arusha, kila mwenye macho ameona, mwenye masikio amesikia.Miradi ya wanasiasa na wafanyabiashara wenye uhusiano wa karibu na wanasiasa wamekuwa na amri juu ya vyombo vya dola kuua mlalahoi yoyote ambaye anataka kuleta kizuizi katika miradi yao isiyohalali, ambayo inamanufaa kwao binafsi na chama chao. Kwa mantiki hiyo kiongozi wa nchi yupo tu kwa mujibu wa katiba lakini nchi hii imeshamilikiwa kwa watu wachache wenye nguvu ya kiuchumi.
Kama inafikia mahali mtu binafsi anaweza kutoa pesa ili chama kiweze kuendelea kukaa madarakani, na baada ya hapo serikali iliyoundwa na chama kilichotumia pesa za mtu huyo, kutengeneza mazingira ya kifisadi kumlipa mtu huyo kwa kutumia kodi za watanzania, unataka kuniambia nchi haijamilikishwa kwa watu binafsi wenye nguvu ya kiuchumi uliyotokana na wizi wa kodi za watanzania.
Ninamshukuru Mkuu wa nchi mstaafu wa awamu ya tatu. Aliweza kuweka mizizi ili kuikwamua Tanzania kutoka katika dimbwi la umaskini. Mfano kuinua tanzania kielimu, alianzisha vyombo kama MMEM,MMES,MMEMKWA. Lakini katika awamu hii hatuoni vyombo hivi vikiendelezwa na kuleta tija kwa watanzania. Waalimu wanahitimu masomo yao wanakaa mtaani miezi kumi huku shule zikiwa hazina waalimu. Kwa mwendo huu hatutafika.
Watanzania tuamke kutoka usingizini nchi hii ni yetu, tusiachie viongozi wanenepesh matumbo yao kwa kutumia kodi zetu.